BRAZIL YAISAMEHE TANZANIA MABILIONI YA FEDHA YA 1979
Serikali ya Brazil imeisamehe Tanzania deni Dola 203milioni ambazo sawa Bilioni 445 ambalo limetokana na mkopo uliotolewa kwaajili ya ujenzi wa barabara ya Morogoro-Dodoma mwaka 1979.
Balozi wa Tanzania Nchini Brazil Dk Emmanuel Nchimbi amesaini mkataba huo kwaniaba ya Tanzania huku Wakili wa Hazina ya Taifa Dk Sonia Portella Nunes akisaini kwa niaba ya Serikali ya Brazil.
Balozi Nchimbi ameishukuru Serikali ya Brazil kwa msamaha huo ambao amesema umeunga mkono jitihada za Rais Dk. John Magufuli kujenga uchumi imara wa Tanzania.
Balozi Nchimbi pia ameuhakikishia Serikali ya Brazil utayari wa Tanzania katika kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na uchumi na Brazil.
Hivyo kuanzia sasa kampuni za Brazil zinaruhusiwa kukopa katika Benki za Brazil kwa ajili ya kutekeleza miradi nchini Tanzania lakini pia Serikali ya Tanzania inaruhusiwa kuanzisha majadiliano ya miradi mipya ya maendeleo.
POLISI ANAYEJIITA FARU JOHN ATAKIWA KWA KAMANDA MAMBOSASA
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amemuagiza Kaimu Kamanda wa Mkoa wa Temeke kuhakikisha askari anayejiita Faru John anafikishwa ofisi kwake kuhojiwa akituhumiwa kwa rushwa.
Agizo hilo amelitoa leo Jumapili baada ya wakazi wa Mbagala kumlalamikia wakidai askari huyo amekuwa akiwakamata wafanyabiashara na kudai kwa nguvu rushwa ya Sh20,000.
Wananchi hao wamelalamika kuwa, mfanyabiashara ambaye hatoi fedha hizo hufungwa pingu na kuzungushwa usiku kucha akiwa kwenye gari la polisi.
Kamanda Mambosasa aliyekuwa akisikiliza kero za wananchi wa Mbagala Zakhem amesema Jeshi la Polisi haliwezi kuwa na askari anayejipa jina la mzaha, huku akiwakandamiza wananchi.
Amesema huo ni mmomonyoko wa maadili kwa askari ambao kazi yao ni kulinda raia na mali zao, hivyo atawachukulia hatua wote watakaobainika kuomba na kupokea rushwa.
"Ninawaomba askari kuwalinda wafanyabiashara wenye mitaji midogo kama vile wakaanga chipsi. Kuwadai Sh20,000 eti kwa sababu wamechelewa kufunga biashara hilo sikubaliani nalo hata kidogo, lazima niwachukulie hatua," amesema Kamanda Mambosasa.
Pia, amekemea askari wanaodai rushwa kwenye vituo vya polisi ambavyo amesema vipo kwa ajili ya kutoa huduma.
Amewaagiza wakuu wa vituo kuhakikisha watu hawakai muda mrefu vituoni kwa kuwa kufanya hivyo ni kutengeneza mazingira ya kupokea rushwa.
Mkazi wa Mbagala, Thabiti Mohamed alisema kuna askari anayejulikana kwa jina la Faru John amekuwa akiwakamata wafanyabiashara, wakiwemo wauza chipsi ambao huchelewa kufunga maduka hadi saa tano usiku na huzunguka nao usiku kucha wakiwa wamewafunga pingu.
Mohamed alisema askari hao huomba kwanza Sh20,000 ili kuwaachia na wasipozitoa ndipo hufungwa pingu na kupakiwa kwenye gari.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Kibangulile, Mashaka Selemani amemuomba Kamanda Mambosasa kuwahamisha askari wa Kituo cha Polisi Maturubai akisema hawakamati wahalifu bali wapo kwa ajili ya kupokea rushwa.
"Askari hawa kazi yao wanapomkamata mtuhumiwa wanampeleka ofisi ya Serikali ya Mtaa Mikwambe, wanapofika kazi yao wanataka fedha kwa nguvu. Wasipopata wanawapiga na kuwabambikia kesi. Tumefuatilia wanakusanya hadi Sh1 milioni kwa siku, hivyo wameshazoeleka tunataka waondolewe Mbagala," alisema Selemani.
POLISI WAMSAKA DEREVA WA LISSU
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto amemtaka dereva wa Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema)Tundu Lissu, ajitokeze ili aweze kutoa maelezo yake kuhusiana na tukio la kupigwa risasi bosi wake.
Kamanda huyo amesema kwamba sababu ya kumtafuta dereva huyo aliyemtaja kwa jina la Adam ni kwa sababu alikuwa pamoja na majeruhi wakati tukio hilo linatokea.
Pia Kamanda huyo alimtaka Katibu Mkuu wa Chadema Dk Vicent Mashinji kufika kwa RCO mjini Dar es Salaam ama Dodoma kutokana kauli yake kuwa katika uchunguzi wao wamewabaini wahusika.
Kamanda Muroto amesema Polisi Mkoani Dodoma wamekamata magari nane aina ya Nissan Patrol kwa ajili ya uchunguzi wa tukio la kupigwa kwa risasi kwa mbunge wa Singida Mashariki (Chadema)Tundu Lissu.
Kamanda Muroto amesema uchunguzi huo unafanywa kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA).
"Uchunguzi wa awali umeonyesha kuwa wahalifu walikuwa na silaha ya SMG/SAR kutokana na maganda ya risasi yaliyokutwa eneo," amesema.
SAKATA LA ALMASI LAENDELEA KUFUKUTA
Kama ulidhani kimbunga kilichotokana na ripoti ya uchunguzi wa biashara ya madini ya almasi na Tanzanite kimemalizika kwa kuwang’oa vigogo kama mawaziri na makatibu wakuu umekosea. Kimbunga hicho kimeendelea kukusanya msururu wa watu na sasa kinaelekea kwa watendaji wengine ambao wapo hatarini kupoteza ‘utajiri wao’.
Ikiwa siku mbili baada ya ripoti hiyo kumng’oa Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Tamisemi, George Simbachawene na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Edwin Ngonyani, naye Waziri wa Fedha Philip Mpango ameagiza watendaji wote walioko katika mgodi wa almasi wa Mwadui Nyinyanga kuchunguzwa na itakapobainika wanamiliki mali zisizoelekeza wachukuliwe hatua.
Waziri Mpango akizunguza wakati alipopokea ripoti kuhusu shehena ya almasi iliyozuiliwa katika Uwanja wa Mwalimu Julius Nyerere amesema ‘Tanzania imepigwa vyakutosha’ hivyo wale wote waliohusika katika upigaji huo washughulikiwe.
Ameviagiza vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na idara za sheria kuanza kuwachunguza wafanyakazi wa mgodi huo kama walihusika kwa njia yoyote kufanikisha utoroshaji wa rasilimali za taifa.
Amesema wafanyakazi wote wanaohusika kuanzia uchimbaji wa madini hayo mpaka kule yanakosafirishwa wamulikwe na vyombo vya dola ili kubaini uhalali wa mali wanazomiliki.
“Vyombo nataka kuanzia sasa wachunguzeni wafanyakazi ambao walishiriki katika kufanikisha kutorosha almasi zetu tena wachunguzeni kwa kina ...angalieni mali zao ikiwa wana mashamba, magari, majumba, viwanja changanyeni,” amesema.
Waziri huyo ambaye kila mara alikuwa akirejea neno ‘Watanzania tumepigwa vyakutosha ...Nataka Watanzania wajue mali zao’ alisema baadhi ya watumishi kwenye mgodi huo walishirikiana na wajanja wa nje kutorosha rasilimali za taifa.
“ Nasema wachunguzeni na kisha wachukuliwe hatua kuanzia wale waliopo sasa na hata wale waliokuwepo nyuma...lakini kama kuna mtu ametangulia mbele ya haki huyo basi,” amesema.
Kauli ya Waziri Mpango imekuja siku mbili tu baada ya Rais John Magufuli kukabidhiwa ripoti ya kamati iliyoundwa na Spika wa Bunge Job Ndugai ambayo ilichunguza biashara ya madini ya almasi na Tanzanite na kubaini madudu kadhaa.
Ripoti hiyo imewataja vigogo kadhaa kuhusika katika uzembe na kulisababishia taifa hasara hatua ambayo ilimlazimu Rais Magufuli kuwataka wakae pembeni kupisha uchunguzi. Juzi akizungumza na waandishi wa habari Mkuu wa Jeshi la Polisi(IGP) Simon Sirro amesema tayari baadhi ya wale waliotajwa kwenye ripoti hiyo wameanza kushughulikiwa na akawataka wengine wanaohusika kujitokeza haraka iwezekavyo.
Kuhusu almasi iliyozuiliwa katika uwanja wa ndege wa JKN, aliyekuwa mwenyekiti wa kuchunguza makinikia yanayozuiliwa katika Bandari ya Dar es Salaam, Profesa Abdulkarim Mruma alisema thamani iliyotolewa na wasafirishaji wa mzigo huo ilikuwa ya uwongo.
Amesema kulingana na tathmini waliyofanya Tanzania ilikuwa ikipoteza mamilioni ya fedha kila mwaka kwa vile vipimo vilivyokuwa vikitumika kuthamini almasi hiyo vilikuwa haziendani na ukweli.
Akirejea yale yaliyoelezwa na Profesa Mruma, Waziri Mpango alisema kutokana na udanganyifu huo Tanzania ilikuwa ikipoteza kiasi cha 2.3 bilioni kama sehemu ya tuzo ya ada na mrahaba. Amesema mbali na hilo kiasi kingine cha fedha kilikuwa kikipotea kutona na wajanja hao wachache kutumia njia za panya kuibia Serikali.
“Tumepigwa kiasi kikubwa kwa maana hiyo kuanzia sasa mapendekezo yote yaliyotolewa na Profesa Mruma yafanyiwe kazi na naagiza watafutwe wataalamu tena wazalendo ili kuziba mapengo yaliyopo,” amesema.
Baadhi ya maofisa wa ulinzi na usalama pamoja na taasisi ya kupambana na kuzuia rushwa( Takukuru) waliokuwepo kwenye mkutano huo walisema operesheni ya kuwachunguza wafanyakazi hao tayari imeanza kufanyika na hadi sasa wafanyakazi kadhaa walikuwa wakihojiwa.
BALOZI: NILISHUHUDIA KICHWA KIKIUNGUA MOTO KWA MGANGA
Balozi wa Nyumba 10 katika Kitongoji cha Chang’ombe Kijiji cha Chamwino Ikulu, Simango Asheri amesema alishuhudia mwili wa Mariam Said (17) anayedaiwa kuuawa nyumbani kwa mganga wa kienyeji, Ashura Mkasanga (33) ukiwa utupu, umetenganishwa kichwa na kiwiliwili huku ukiingua moto kichwani.
Mauaji hayo yalitokea Agosti 8 mwaka huu saa 10 usiku, umbali wa kilometa mbili kutoka mahali ilipo Ikulu ya Chamwino mkoani hapa.
Akizungumza nyumbani kwake hivi karibuni Asheri alisema wakati akiwa anafanya shughuli zake za ujenzi nyumbani kwake saa 3 asubuhi alipita mwenyekiti wa tawi la CCM akamweleza kuhusu tukio hilo.
“Akaniambia kuna mtu kafa kwa Malita Mkasanga (Ashura), tukakimbia (kwenda) mwenzangu alikuwa na baiskeli mimi nilikuwa peku, tukafika tukakutana na wazee wamekaa tukakaribishwa nendeni mkaangalie tukio,” anasema.
“Tulipofika ndani tukakuta mtu amelala chali sebuleni kuangalia tukaona moto unaendelea kufuka kichwani, alikuwa hana nguo, tulitoka lakini baada ya muda tuliingia tena kutazama tukakuta shingo imesogezwa kwa kukatwa,” anasema.
Balozi huyo anasema walipomuuliza Ashura ilikuaje hadi mtu huyo akafia nyumbani kwake, aliwaambia kuwa akiwa amelala ndani mtoto wake wa kiume alisikia kelele nje.
“Alituambia kuwa marehemu alipiga mlango na kuingia ndani na kudondoka sebuleni huku moto ukaendelea kuwaka, tuliendelea kumuhoji kama mlango uliokuwa umefungwa aliupiga na kuingia ndani mbona ni mzima haukuvunjika, alijibu hata yeye anashangaa,” anasema.
Alipobanwa na wazee wa kijiji kuhusu ni wapi majivu yaliyokuwa ndani ya nyumba hiyo yalipotokea, aliwajibu kuwa hata yeye anashangaa kwa sababu hajui yalipotoka.
“Alipoulizwa kuhusiana na mchanga uliokuwepo ndani ya nyumba hiyo, pia alijibu anashangaa ulipotokea. Kutokana na majibu hayo tulimwacha tukiwasubiri polisi waje,” anasema.
Asheri anasema kuwa pembeni mwa mwili wa marehemu kulikuwa na lundo la mchanga ambalo baada ya kufukuliwa ilibainika kuwa chini kulikuwa na damu iliyofukiwa.
Uhalali wa kazi ya mganga
Hata hivyo, balozi huyo anapoulizwa iwapo alikuwa anafahamu kuwa Ashura alikuwa mganga wa kienyeji, anasema hafahamu na kwamba watu wanaofanya shughuli hizo kijijini hapo wote wanajulikana.
“Wanasema kuwa ni mganga, lakini mimi tangu amehamia hapa miaka mitano hivi namfahamu kama mkulima na mumewe anafanya kazi katika gari moja la kusombea mchanga huko,” anasema.
Badala yake anasema kuwa Ashura alikuwa akishiriki vizuri shughuli za jamii yake kwa kuchanga michango mbalimbali na kushiriki kwenye mikutano ya kitongoji na kijiji.
Ndugu wachukua watoto
Mjomba wa mumewe wa mganga huyo ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, anasema baada ya tukio hilo polisi waliwachukua watu wote waliokuwepo ndani ya nyumba hiyo wakiwemo watoto.
“Lakini baadaye tuliambiwa kuwa watoto wameachiwa wamerudi nyumbani, tukaamua twende tukawachukue ili ndugu wa marehemu wasije wakawadhuru,” anasema.
Anasema watoto hao walipelekwa kwa bibi yao na wataishi huko hadi wazazi wao watakapomaliza matatizo yaliyojitokeza.
“Huyu ndugu yetu awali alikuwa akiishi na dada yangu, lakini walikuwa hawaelewani kwasababu mama yake alikuwa akimwambia aachane naye kwasababu ni mshirikina lakini alikataa,” anasema.
Anaongeza kuwa baada ya muda walinunua shamba na hivyo kuondoka kwa mama yake na kwenda kuanzisha mji wao.
Hata hivyo, mmoja wa watoto wa mganga huyo, (jina tunalihifadhi), anasema kuwa siku ya tukio hakulala nyumbani.
“Niliporudi nyumbani asubuhi ndiyo nilikutana na tukio hilo wala sikufahamu ilikuaje,” anasema mtoto huyo ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha pili katika moja ya shule wilayani humo.
Nyumbani kwa mganga
Mazingira ya nyumba hiyo ambayo ipo umbali wa takriban mita 300 kutoka kwa majirani zake, yamegubikwa na utulivu mkubwa huku milango ikiwa imefungwa.
Nje ya nyumba hiyo iliyojengwa kwa matofali ya udongo kuna kisima kilichochimbwa kienyeji kikiwa na maji machache, mabua ya mtama uliovunwa na pembeni kukiwa na nyumba iliyoanza kujengwa kwa matofali ya saruji.
Inaelezwa kuwa katika nyumba ya jirani kuna mzee anaishi lakini hata hivyo wakati mwandishi wa habari hizi, anafika hakukuwa na mtu.
Hata hivyo, tofauti na matukio mengine hakuna kiongozi wa kijiji hicho cha Chamwino Ikulu aliyekuwa tayari kuelezea tukio hilo kwa sababu mbalimbali.
Waganga wazungumza
Akizungumza hivi karibuni mmoja wa waganga wa tiba asilia mjini hapa, Dk Harun Kifimbo anasema Serikali ihakikishe mipango inayopangwa kudhibiti watu wanaojifanya waganga wa tiba asilia inasimamiwa.
“Tatizo pia liko kwa baadhi ya waratibu wanaotoa vyeti kwa waganga wasiostahili na ndiyo wanaofanya mambo haya ambayo yanaenda kinyume na tiba ya asili,” anasema Kifimbo.
Anasema chama cha waganga wa tiba asili mkoani Dodoma kimepanga kuendesha msako na kuwakamata watu wanaojishughulisha na tiba hizo bila kuwa na leseni, cheti cha kuthibitishwa mahali wanapofanyia kazi zao na dawa zao kutokuwa na usajili kwa mujibu wa sheria.
Hata hivyo, anawalamu baadhi ya waganga kuwa wamekuwa wakijiharibia mambo yao wenyewe kwa kufanya mambo ambayo yanakatazwa kisheria wakati Serikali imewawekea mazingira mazuri ya kufanyia kazi.
Polisi waendelea na uchunguzi
Aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa ambaye sasa amehamishiwa Dar es Salaam, alisema waliwakamata watuhumiwa 11 na kuwahoji, kati yao watano wanaendelea kuwa chini ya ulinzi.
“Kule Chamwino wanamamlaka ya kuwafikisha mahakamani wakimaliza uchunguzi wao,” anasema.
Mambosasa alisema jumla ya watu 11 walikamatwa katika tukio hilo ambalo Mariam aliuawa kwa kukatwa shingo yake na kutenganishwa na kiwiliwili na kuchomwa moto kichwa chake na kubakia vufu lisiloweza kutambuliwa sura yake.
“Baadhi ya sehemu za mwili wake ziliunguzwa kwa moto ambazo ni mkono wa kushoto, shingo, kifuani na sehemu za siri,” alisema.
Alisema mazingira ya tukio hilo yanaonyesha kuwa mganga huyo asiyekuwa na kibali cha kuendesha shughuli za tiba asili analaza wagonjwa nyumbani kwake, anafanya matambiko, anapiga ramli chonganishi na anafanya tohara.
“Katika nyumba yake alikutwa kalaza watu wanane kati yao wanawake sita na wanaume wawili,” anasema.
Hata hivyo, anasema hakuna maelezo ya kutosha jinsi gani marehemu alifika kijijini hapo kutoka Kigoma na kwamba polisi inafanya uchunguzi zaidi wa tukio hilo.
“Tukio hili halikubaliki hapa Dodoma na mahali popote ni fedheha kubwa sana kwa wanachamwino kuendelea kukumbatia ushirikina katika karne hii na Serikali imesogeza huduma za afya karibu na jamii, lakini bado hawataki kwenda kutibiwa hospitali na kukubali kuuawa kwa fedheha na waganga wachonganishi wa jadi,” anasema.
SAKATA LA MIMBA SHULENI LATUA KWA MA-DC
Lile sakata la ujauzito sasa limeshuswa kwa wakuu wa wilaya baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuwataka kusimamia utekelezaji wa sheria za nchi zenye lengo la kumlinda mtoto wa kike na mimba shuleni.
Majaliwa amewataka wabunge kushirikiana na halmashauri zao katika kuweka mikakati ya kudhibiti ujauzito kwa watoto wa shule.
“Wahamasisheni wananchi watoe ushirikiano kwa vyombo vya dola ili wanaowapa ujauzito au kuwakatisha masomo waozeshwe wapate adhabu stahili,” amesema Majaliwa kabla ya kuahirishwa kwa Bunge.
Amesema dhamira ya Serikali ni kumlinda mtoto wa kike ili apate elimu kwa ajili ya manufaa yake na Taifa kwa ujumla.
“Kila Mtanzania ana wajibu wa kuhakikisha watoto wetu wanapata elimu. Hivyo ni lazima tuhakikishe mtoto wa kike anapata elimu stahiki na masomo yake hayakatizwi kwa kupata ujauzito,” amesema.
Alisema kwa mujibu wa kifungu cha Sheria ya Elimu Sura ya 353 kinatoa adhabu ya miaka 30 jela kwa yeyote atakayeoa au kumpa ujauzito mwanafunzi.
“Kuwaachisha masomo wanafunzi waliopata ujauzito ni utekelezaji wa Waraka na Kanuni za Elimu za Mwaka 2002 zinazohusu kufukuzana kuondoa wanafunzi shuleni kutokana na makosa mbalimbali ikiwemo uasherati, wizi kutumia dawa za kulevya,” amesema na kuongeza kuwa; “Pamoja na utoro unaotokana na baadhi ya wanafunzi kwenda kufanya shughuli za biashara ndogo ndogo kucheza kamari, kuvua samaki, kuchimba madini.”
JINO KWA JINO MISWADA YA RASILIMALI
Baada ya kuzisaidia nchi za kusini mwa Afrika kupata uhuru wake, Tanzania inaonekana sasa kuliongoza bara hili kwenye mapambano ya uhuru wa kiuchumi.
Hii ndiyo imani iliyopo miongoni mwa baadhi ya wabunge waliojadili miswada mitatu iliyowasilishwa kwa hati ya dharura na kuridhiwa bungeni wiki hii.
Wengi wanakumbuka, baada ya Tanzania kupata uhuru wake haikuridhika kuona majirani zake wanaendelea kukaliwa na wakoloni, hivyo ilihakikisha inatoa msaada wa hali na mali kuhakikisha Waafrika wote wanakuwa huru.
Licha ya uhuru huo wa bendera, bado mataifa mengi hayanufaiki na rasilimali nyingi zilizomo ndani ya mipaka yao huku mataifa ya magharibi yakionekana yananeemeka zaidi.
Takwimu zinaonyesha kwamba, kiasi ambacho Afrika inapokea kupitia misaada ya maendeleo na mikopo nafuu ni sehemu ndogo ikilinganishwa na kiasi inachopoteza kutokana na mfumo wa ukwepaji kodi, uongezaji wa gharama za ununuzi pamoja na uvunaji rasilimali za aina mbalimbali.
Ujangili, uvunaji na usafirishaji haramu wa magogo pamoja na uchimbaji wa madini bila kuwanufaisha wananchi wa mataifa husika ni miongoni mwa changamoto zinazoikabili Afrika, hivyo kudumaza uchumi wake.
Hata hivyo, miswada mitatu iliyowasilishwa kujadiliwa na kupitishwa bungeni Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe alisema kuwa zinaifanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza kuanza kupigania rasilimali zake.
Akiwataka wabunge wenzake kuijadili miswada ya mamlaka ya nchi kuhusiana na umiliki wa maliasili na ule wa mapitio na majadiliano kuhusu masharti hasi katika mikataba ya maliasili za nchi bila kuweka ushabiki wa vyama vyao, Zitto anasema mabadiliko hayo yanahitaji ushirikiano wa Watanzania wote.
“Tanzania tumekuwa nchi ya kwanza Afrika kuliweka suala hili kwenye sheria zetu, kwamba chochote kilichopo juu au chini ya ardhi yetu, ni chetu,” alikumbusha kiongozi huyo wa Chama cha ACT-Wazalendo.
Msimamo wa Zitto unafanana na wa mwenzake wa Kigoma Kaskazini, Peter Serukamba anayemtaka Waziri wa Katiba na Sheria kuhakikisha anasimama kidete kwenye vita hii na kutokubali kuyumbishwa na mataifa au mashirika makubwa ya kimataifa ambayo yataathirika na mabadiliko haya.Kwa kutambua kwamba ‘wakubwa’ hao watakasirika kwa maamuzi haya, Serukamba anasema: “Bunge litakuwa limeweka historia ambayo haitasahaulika kwa vizazi vijavyo.”
Nguvu kwa Rais
Muswada unampa mamlaka Rais wa Tanzania kusimamia rasilimali zote zilizopo kwa niaba ya Watanzania, jambo ambalo baadhi ya wabunge wa upinzani wanadhani ni madaraka makubwa yanayopaswa kupunguzwa.
Mbunge wa Kibamba, John Mnyika anatahadharisha kwamba endapo itatokea wakati wowote Tanzania itakapompata Rais mwingine ambaye hana uzalendo kama unaoonyeshwa na Dk John Magufuli huenda akayatumia vibaya madaraka hayo.
Kuepusha hilo, anashauri, “Serikali iruhusu kuendelezwa kwa mchakato wa Katiba Mpya iliyopendekezwa na Jaji (mstaafu Joseph) Warioba ambayo inapunguza madaraka ya Rais.”
Akibainisha mapungufu yaliyomo kwenye miswada iliyopitishwa, anasema mwaka 2008 wakati wa mjadala wa sakata la akaunti ya Tegeta Escrow, kulikuwa na azimio la kuzitaka kamati za Bunge za kisekta zipewe mikataba na Serikali kabla haijaridhiwa, jambo ambalo halijatekelezwa mpaka leo.
Licha ya ukweli huo, Mnyika anasema: “Hata sasa, mapendekezo haya hayasemi chochote kuhusu mikataba hiyo kuletwa bungeni kabla haijasainiwa.”
Mnyika anaungwa mkono na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema anayesema kuwa ushabiki katika utungaji wa sheria umekuwa ukipewa nafasi kubwa tofauti na inavyotakiwa.
Mbunge huyo anaeleza kusikitishwa na mpango wa kuiwasilisha miswada hiyo mitatu kwa hati ya dharura.
Lema anakwenda mbali ana kutaka kinga ya viongozi wawapo madarakani iondolewe ili waweze kuwajibishwa wakati wowote watakapothibitika kufanya mambo yaliyo nje ya majukumu yao na kulisababishia taifa hasara.
“Kwa madaraka anayopewa Rais, ikitokea akaja mwingine huenda ikawa kutoka upande wetu ambaye atakuwa tofauti na Rais Magufuli, atakuja kuliuza Taifa hili. Hatutungi sheria kwa kuzingatia Rais aliyepo madarakani, bali kwa kuzingatia uwezekano wa masuala kadhaa kutokea,” anaonya Lema, japokuwa angalizo lake halikupata muungaji mkono. Kana kwamba haitoshi, mbunge huyo anawataka wabunge wenzake kutunga sheria ambayo hata hapo baadaye kama hawatakuwapo bungeni basi zitawakulinda.
“Kutokumwamini Rais siyo jambo zuri hata kidogo lakini kwa asili ya mataifa ya Afrika tunahitaji kuchukua tahadhari,” anasisitiza Lema.
Kutokana na hoja hizo, Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi alifafanua kwanini Rais anapewa mamlaka hayo na kuwatoa uoga wabunge juu ya uwezekano wa kuyatumia vibaya wakati wowote.
Katika kujenga hoja yake, Profesa Kabudi anatoa mfano wa Ethiopia, India na Uingereza ambako marais wao si watendaji, lakini wamepewa mamlaka juu ya rasilimali zote za mataifa yao. Anasema hata mataifa makubwa kama Marekani suala hilo liko hivyo.
Endapo itatokea Rais akapotoka huko mbeleni, anasema: “Katiba yetu imeweka mifumo ya kudhibiti madaraka za kutosha kuhusu madaraka ya Rais wetu ikiwamo kupigiwa kura ya kutokuwa na imani naye. Kwa hiyo, hilo halinipi shida.”
Kwa kuzingatia kwamba muswada hauna ubishi katika eneo lolote isipokuwa kutokana na itikadi za kisiasa, waziri huyo anasema wabunge wote wanapaswa kusimama pamoja na kusema wamelitendea haki taifa hili.
“Ubishi unaojitokeza upo kwenye mawanda ya kisiasa. Hakuna mbunge hata mmoja ambaye hauungi mkono muswada uliopo.
Michango mingi iliyotolewa imekuwa ni ya kujenga na kuboresha ili tufikie muafaka mwema,” anasema Profesa Kabudi.
Kwa mujibu wa waziri huyo mabadiliko yaliyofanywa kwenye miswada hiyo, yanaipa Serikali mamlaka ya kuipitia mikataba yote iliyosainiwa ili kuona taifa linanufaika kwa kiasi gani.
Profesa Kabudi anasema utekelezaji wa sheria utahusu mikataba yote iliyopo, ingawa sheria yenyewe itaanza kufanya kazi mara tu baada ya mikataba kusainiwa. “Ni utaratibu uliopo na unatumika sehemu nyingi duniani. Wamarekani wanautumia sana,” anafahamisha.
Maoni ya wadau
Kwa siku mbili mfululizo, kamati za bunge zinazohusika na wizara ya sheria zilikuwa zinapokea maoni ya wadau mbalimbali waliopata nafasi ya kushiriki.
Zilikuwapo kamati mbili; Katiba na sheria iliyokuwa inajadili na kupokea maoni juu ya muswada wa mabadiliko ya sheria mbalimbali pamoja na kamati ya pamoja iliyoundwa kusikiliza hoja za miswada miwili iliyobaki.
Miongoni mwa waliojitokeza ni Katibu Mtendaji wa Chemba ya Nishati na Madini (TCEM), Gerald Mturi ambaye, licha ya mengi aliyoyapendekeza, anasema suala la usuluhishi wa migogoro baina na wawekezaji wa kimataifa na Serikali lisifanywe na mahakama za ndani ili kutopunguza imani yao.
“Kupeleka shauri hilo kwenye mahakama za kimataifa kunaongeza kujiamini kwa wawekezaji. Naomba kipengele kinachotaka mahakama za ndani kusikiliza migogoro hii kiondolewe,” anasema Mturi.
Katika kutekeleza haki hiyo ya kikatiba, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Mawakili Watetezi wa Mazingira (Leat), Dk Rugemeleza Nshala anasema msimamo wa kutumia mahakama za ndani ni mzuri kwani licha ya kuongeza uwezo wa wataalamu wetu, utaimarisha taasisi za haki zilizopo pia.
Kama kutakuwa na mgogoro wowote unaopitiliza uwezo wa mahakama za ndani basi sheria iutambue kuwa ni batili.
“Ikihitajika wataalamu wetu wapelekwe shule kuwajengea uwezo unaotakiwa kuzitendea haki kesi hizo lakini ni lazima ziamriwe nchini,” alisema Dk Nshala.
Upinzani
Kambi rasmi ya upinzani bungeni haikunyamaza. Ilizungumza kila ilipoona ama pana utata au upungufu unaoweza kuliletea Taifa hasara siku za mbele. Akisoma hotuba hiyo kwa niaba ya Waziri Kivuli wa Katiba na Sheria, Tundu Lisuu, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche anasema umakini unahitajika kutekeleza haki ya bunge kupitia mikataba itakayoridhiwa na Serikali.
Anasema licha ya sheria mpya kuruhusu Bunge kupitia mikataba hiyo, bado Serikali imepewa uwezo wa kuingia mikataba hiyo kabla Bunge halijajua chochote, suala ambalo linaweza lisiwe na tija endapo utaratibu huo hautakuwa na mkakati makini.
“Kambi inapendekeza Serikali isiingie mkataba wowote unaohusu rasilimali za nchi mpaka mikataba hiyo itakapojadiliwa na kuridhiwa na Bunge,” anasema Heche.
Licha ya Bunge kuwa na uwezo huo, ilipendekezwa wananchi hasa waliopo kwenye maeneo yenye rasilimali husika washirikishwe kupitia Serikali zao za mitaa, vijiji na vitongoji.
“Wapewe haki ya kushirikishwa, kuhusishwa na kutaarifiwa kuhusu maamuzi ya utafutaji au uvunaji wa rasilimali zilizopo kwenye maeneo yao,” anasema.
Kamati ya pamoja
Ikiongozwa na Mbunge wa Bukombe, kamati hii iliyoundwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai ilitoa mapendekezo yanayotaka kuharakishwa kwa utunzi wa kanuni zake zitakazosaidia utekelezaji wake pindi itakaposainiwa na Rais.
Kufanikisha ama ya kutungwa kwa sheria hiyo, Biteko aliishauri Serikali kuboresha utendaji wa vyombo na taasisi zinazosimamia Sekta ya maliasili ili kuhakikisha rasilimali hizo zinawanufaisha Watanzania na taifa kwa ujumla.
MSHINDI WA KUCHORA NEMBO YA EAC KULAMBA DOLA 25,000
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Kikanda na Kimataifa, imewataka vijana wenye uwezo wa kubuni na kuchora kujitokeza kushiriki shindano la kubuni nembo mpya ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Msemaji wa wizara hiyo, Mindi Kasiga amesema shindano hilo ni fursa kwa vijana kuonyesha uwezo wao, pia kujipatia kipato iwapo watashinda.
Shindano hilo limeanza Juni Mosi na mwisho ni Agosti 31.
“Shindano hili limezinduliwa mwezi uliopita pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Kigezo ni vijana wenye umri kati ya miaka 18 na 35 wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wote wanaruhusiwa kushiriki,” amesema Kasiga leo (Julai 5).
Amesema kuzindulia shindano hilo chuo kikuu haimaanishi kuwa shindano hilo linalenga wanafunzi pekee, bali vijana wote wenye uwezo wa kubuni kwa njia yoyote si lazima iwe ya kompyuta.
“Tunahitaji wajitokeze kwa wingi, hili ndilo linatoa nafasi nzuri ya kushinda, sisi katika jumuiya tunafanya mambo mengi na tuna umuhimu, tuna eneo kubwa kuliko nchi zingine wanachama, makao makuu yapo huku, vijana wajitokeze ili waweze kupata fedha za ushindi zilizoandaliwa,” amesema Kasiga.
Amesema mshindi wa kwanza atazawadiwa Dola 25,000 za Marekani (Sh55 milioni) wa pili atapewa Dola 5,000 (Sh11 milioni) na wa tatu Dola 2,500 (Sh5.5 milioni).
BAKWATA YALAANI MAUAJI KIBITI
Kaimu Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Salumu Ahmed Abeid amesema baraza hilo linalaani mauaji yaliyotokea hivi karibuni wilayani Kibiti, mkoani Pwani.
Pia, Abeid amesema Bakwata imesikitishwa na vitendo hivyo vya mauaji kwa sababu vinachafua amani ya nchi.
"Baraza Kuu la Waislamu Tanzania linatoa pole kwa wananchi na limesikitiswa na vitendo vinavyotaka kuchafua amani ya nchi hasa vinapohusishwa na Uislam," amesema Abeid leo, Jumatatu wakati akitoa salamu za Bakwata Taifa katika Bazaza la Eid mjini Moshi.
Kutokana hilo Bakwata imeiomba Serikali iongeze umakini katika kushughulikia suala la mauaji mkoani Pwani.
Swala ya Eid na Baraza la Eid, zinazofanyika kitaifa katika msikiti wa Masjid Riadha mjini Moshi mkoani Kilimanjaro.
Sherehe hizo za Sikukuu ya Eid zimehudhuriwa na wageni mbalimbali ikiwa ni pamoja na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ambaye ndiye mgeni rasmi.
Wageni wengine ni pamoja na Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira.
MAJALIWA: MARUFUKU KUSAFIRISHA CHAKULA NJE YA NCHI
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amepiga marufuku usafirishaji wa chakula nje ya nchi bila kibali na kuwataka wafanyabiashara kuuza chakula kwenye maeneo yenye uhaba nchini.
Majaliwa ametoa agizo hilo leo, Jumatatu wakati akihutubia Baraza la Eid katika Msikiti wa Masjid Riadha mjini Moshi mkoani Kilimanjaro.
Waziri Mkuu huyo amesema kuwa kuna maeneo ambayo wananchi hawakupata chakula vizuri kutokana na uhaba wa mvua hivyo wafanyabiashara wapeleke chakula kwenye maeneo hayo.
“Serikali bado haijatoa kibali cha kutoa chakula nje ya nchi, kama unaona kuna umuhimu kaombe kibali, lakini utapewa kibali cha kusaga upeleke unga na siyo mahindi,”amesisitiza Majaliwa.
Majaliwa ameonya kuwa kwa wale watakao kamatwa wakisafirisha mahindi nje ya nchi kinyume na utaratibu, mahindi hayo yatataifishwa na kupelekwa kwenye ghala la Taifa na magari yatapelekwa polisi.
Amesema kuwa Serikali imepokea barua za maombi ya kupeleka chakula nchi jirani, lakini bado haijatoa ruhusa.
RAIS MAGUFULI KUFUNGUA VIWANDA MKOANI PWANI
Rais John Magufuli leo (Jumanne) anaanza ziara ya kikazi ya siku tatu mkoani Pwani.
Taarifa ya Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa, iliyotolewa jana (Jumatatu) kwa vyombo vya habari imesema katika ziara hiyo, Rais atazindua viwanda vikubwa vitano.
Viwanda hivyo vimetajwa kuwa ni cha vifungashio (Global Packaging Co. Ltd), cha matrekta (Ursus- Tamco Co. Ltd), cha chuma (Kiluwa Steel Group), cha kukausha matunda (Elven Agric Company) na cha vinywaji baridi (Sayona Fruits).
Msigwa amesema Rais pia atazindua mradi wa maji wa Ruvu na Barabara ya Bagamoyo- Msata.
Taarifa imesema Rais Magufuli katika ziara hiyo atakutana na kuzungumza na wananchi katika mikutano ya hadhara iliyoandaliwa.
KAMUSI KUU YA KISWAHILI YAZINDULIWA
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali inatambua umuhimu wa lugha ya Kiswahili kwa ustawi wa Taifa na katika kulinda umoja wa kitaifa.
Ametoa kauli hiyo jana (Jumatatu) alipozungumza na wabunge, viongozi wa Serikali na wananchi waliohudhuria uzinduzi wa Kamusi Kuu ya Kiswahili uliofanyika kwenye ukumbi wa Bunge mjini Dodoma.
“Serikali inatambua umuhimu wa lugha ya Kiswahili kwa ustawi wa nchi yetu na katika kulinda umoja wa kitaifa. Hakika lugha ya Kiswahili ndiyo inayotufanya tuwe Watanzania. Hivyo, tunaithamini na kwetu hii ni lulu na tunu ya Taifa,” amesema.
Waziri Mkuu katika taarifa iliyotolewa na ofisi yake amesema uzinduzi wa kamusi hiyo unaenda sambamba na azma ya Serikali ya kutumia Kiswahili kwenye shughuli zote za kitaifa kama vile mikutano, mijadala, semina na ufundishaji shuleni.
Majaliwa amempongeza Rais John Magufuli kwa kuhimiza matumizi ya Kiswahili kwenye mikutano na matukio muhimu ya kitaifa, kama vile dhifa za kitaifa anazowaandalia wageni wake kutoka nje.
“Hata alipokuwa kwenye mkutano wa wakuu wa nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika, Rais alitumia Kiswahili kuhutubia mkutano huo. Amekuwa akifanya hivyo, hata kwenye mikutano ya Jumuiya ya Afrika Mashariki lengo lake ni kuitangaza lugha hii ya Kiswahili,” amesema.
Amewasihi wazazi wahakikishe watoto wao wanapata kamusi hiyo kama moja ya nyenzo zao za kujifunza lugha ya Kiswahili.
“Ninashauri makundi mengine kama vile waheshimiwa wabunge, wanahabari, wakalimani, wafasiri, waandishi na wahariri wa vitabu, maofisa mawasiliano wa kwenye ofisi zetu, muone umuhimu wa kununua kamusi hii ili iwasaidie kujiimarisha kwenye matumizi ya Kiswahili fasaha na sanifu,” amesema.
Awali, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe amesema Kiswahili ni lugha ya pili inayotumiwa na watu wengi zaidi barani Afrika lakini pia ni lugha ya 10 kati ya 6,000 zinazozungumzwa na watu wengi duniani.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita), Dk Seleman Sewangi amesema kazi ya kuandaa kamusi hiyo ilianza Agosti 12, 2011 na kukamilika mwaka 2015 na toleo la kwanza lilichapishwa.
Amesema kamusi hiyo imekusanya maneno mengi makuu (vidahizo) kuliko kamusi zilizotangulia na kwamba ya sasa ina maneno 45,500.
HIZI NDIZO FEDHA AMBAZO TANZANIA INGEPATA KWENYE MAKONTENA 277
Baada ya kamati ya uchunguzi wa makinikia ya madini kutoa ripoti yake juzi, wengi wanaona kuwa Tanzania imekuwa ikiibiwa kiasi kikubwa cha fedha tangu usafirishaji mchanga wa dhahabu ulipoanza takriban miaka 20 iliyopita.
Wako wanaosema kuwa kiwango hicho cha fedha kinachotokana na kati ya tani 7.8 hadi 15 za madini yaliyo katika makinikia hiyo, kingeweza hata kutosheleza mahitaji ya bajeti ya mwaka.
Lakini kwa mujibu wa kanuni za uchimbaji madini, stahiki ya nchi katika madini haiwezi kuzidi asilimia 10 ya mrabaha.
Kamati iliyoundwa na Rais ambayo iliongozwa na Profesa Abdulkarim Mruma, ilisema imebaini kuwa kampuni ya Acacia, ambayo inaendesha migodi mitatu nchini, haikutangaza madini yote yaliyomo kwenye mchanga huo uliozuiwa bandarini na kwamba kiwango cha dhahabu iliyomo ni kubwa zaidi ya kilichotangazwa.
Wachimbaji wa madini wenye leseni pamoja na kulipa kodi nyingine kwa Serikali kama za mapato na kampuni, hutakiwa na Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 kulipa mrabaha.
Mrabaha ni malipo yanayofanywa na kampuni inayochimba madini kama fidia ya kiuchumi inayolipwa kwa Serikali kutokana na kuchimba rasilimali zake ambazo hazina mbadala.
Kwa mujibu wa kifungu 87(1) wachimbaji wa urani, almasi ghafi na vito ghafi wanatakiwa kulipa mrabaha wa asilimia tano huku kwa madini kama dhahabu, shaba, fedha na platina wakitoa asilimia nne ya thamani ya madini yote.
Madini mengine ya ujenzi kama mchanga, mawe, chokaa hutakiwa kulipiwa mrabaha wa asilimia tatu wakati vito vilivyokatwa na kuchongwa vikilipiwa asilimia moja.
Matokeo ya kamati yanaonyesha kuwa thamani ya madini yote yaliyopo kwenye makontena 277 ni kati ya Sh829.4 bilioni hadi Sh1.439 trilioni.
Iwapo hesabu ya asilimia nne ya mrabaha itapigwa kwa thamani ya chini iliyoanishwa na kamati ya Sh829.4 bilioni kwa kuzingatia dhahabu, fedha na shaba zina thamani kubwa kuliko madini mengine yaliyoanishwa, basi Serikali ilitakiwa ipate Sh33.17 bilioni.
Ripoti ya kamati ya Profesa Mruma ilijumuisha hesabu za madini yote yenye thamani katika makontena hayo yakiwemo yale ya kimkakati kama lithium inayotumika zaidi duniani kutengeneza betri za vifaa vya kielektroniki kama simu za mkononi.
Na iwapo asilimia hiyo nne itapigwa kwa kiwango cha juu cha thamani ya madini hayo cha Sh1.439 trilioni, Serikali ilitakiwa ipate mrabaha wa Sh57.56 bilioni.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa nyaraka zilizotolewa na wazalishaji zilionyesha makontena hayo yalikuwa na dhahabu tani 1.1 yenye thamani ya Sh97.5 bilioni.
Lakini Acacia katika moja taarifa zao za hivi karibuni juu ya ufafanuzi kuhusu makinikia wanaeleza kuwa kontena moja la tani 20 lina thamani ya wastani wa Sh310 milioni. Hii ina maana kuwa mzigo wote uliomo kwenye makontena 277 una thamani ya Sh85.87 bilioni.
Kwa hesabu za Acacia ambazo zinajumuisha madini ya dhahabu, fedha na shaba pekee, Serikali ilitakiwa kupata mrabaha wa Sh3.43 bilioni. Kampuni hiyo inapinga kuwa madini mengine yaliyosalia yaliyoorodheshwa na kamati hayana thamani ya kibiashara.














0 comments:
Post a Comment