SEKTA YA BENKI YAANZA KUONA NURU MPYA

ISM YATOA UFADHILI KWA WANAFUNZI 8 NJE

TIMIZA VIKOBA YAFIKIA VIKUNDI ZAIDI YA 70
Dar es Salaam. Sekta ya benki nchini imeanza kupata matumaini ya kupunguza kiwango cha mikopo isiyolipika kutokana na kuanza kuimarika kwa biashara.
Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Ecobank, Mwanahiba Mzee ameiambia
Mwananchi
katika mahojiano maalumu leo Alhamisi kuwa kwa miaka miwili iliyopita sekta ya benki ilipata misukosuko kidogo kutokana na wafanyabiashara kuyumba lakini sasa kuna mwelekeo chanya.
Amesema sekta ya benki iliyumba kutokana na baadhi ya wafanyabiashara kucheleweshewa malipo ya kandarasi zao na kutofanya vyema kwa baadhi ya sekta muhimu kama ya gesi jambo lililofanya washindwe kurejesha mikopo kwa wakati.
Mzee aliyetembelea ofisi za
Mwananchi
amesema athari zozote zinazowakumba wafanyabiashara zinaathiri pia benki na sekta ya majengo, ambayo sehemu kubwa hutumika kama dhamana ya mikopo.
Mikopo chechefu ni ile ambayo wakopaji wameshindwa kuilipa kwa taasisi za fedha ndani ya muda unaotakiwa ambao ni siku 90.
“Kandarasi nyingi bado hazijalipwa na sehemu kubwa ya dhamana za mikopo hiyo ni majengo ambayo yanashuka thamani kwa sababu wanunuzi ni wachache… hii ni hali ngumu kwa wateja,” amesema.
Amesema benki nyingi hazijapoteza fedha walizokopesha ila ni utaratibu wa kibenki unaofanya zionekane kama ni mikopo isiyolipika ilihali wanaodaiwa watailipa siku zijazo licha ya mdhibiti kutotaka kujua sababu za wateja kushindwa kulipa kwa wakati.
“Sasa hivi hata wasafirishaji waliokuwa wamepaki malori wameanza kupata biashara kwa sababu mambo yameanza kurekebishwa. Malipo ya mikopo yameanza kuja hivyo biashara nyingi zinazidi kuimarika.
“Inawezekana mwishoni mwa mwaka huu bado hali ikawa ngumu kwa sababu ndiyo wanaendelea kuimarika lakini mwakani hali itakuwa nzuri na tutaanza kuona tofauti,” amesema.
Ecobank ni miongoni mwa benki zilizokuwa na kiwango kikubwa cha mikopo chechefu kwa kuwa na asilimia 57 ya mikopo yote katika robo ya kwanza mwaka huu ikilinganishwa na asilimia 38 ya robo ya mwisho wa mwaka jana.
Bosi huyo mpya amesema kazi yake kubwa kwa sasa ni kupunguza kiwango hicho cha mikopo isiyolipika ambayo imekuwa ikiisumbua benki na kuathiri faida ambayo hupatikana katika uendeshaji.
“Malengo ya Ecobank Group ni kuwa na wateja milioni 100 ifikapo 2020 lakini hapa Tanzania nataka tuwe na wateja zaidi ya milioni katika kipindi hicho na kuifanya benki iwe na faida zaidi,” amesema Mzee aliyeteuliwa kuiongoza benki hiyo kuanzia Julai.
ISM YATOA UFADHILI KWA WANAFUNZI 8 NJE
Shule ya Kimataifa ya International School Moshi (ISM), imewatafutia ufadhili wa zaidi ya Sh4.7 bilioni wanafunzi wanane kwenda kusoma nje ya nchi.
Mkurugenzi Mtendaji wa ISM, Bob Horton alisema kwa ufadhili wa mwaka huu unafanya thamani ya jumla ya walionufaika ndani ya miaka mitano iliyopita kuwa Dola milioni nane za Marekani (zaidi ya Sh38.72 bilioni).
Wanafunzi hao watakwenda kusoma katika vyuo vikuu vilivyopo Marekani, Canada na Uingereza. “Mwaka huu tumepata ufadhili wa Dola 2.1 milioni za Marekani (zaidi ya Sh4.7 bilioni) kwa ajili ya wanafunzi wanane, watakaojiunga na vyuo vikuu bora duniani,” alisema Horton. Kozi zinazofundishwa na ISM zinawaandaa wanafunzi kuwa viongozi wa siku zijazo hasa kupitia progamu yake ya diploma ya kimataifa ya Baccalaureate (International Baccalaureate Diploma programme).
Mkurugenzi huyo alisema moja ya malengo ya ISM ni kuwasaidia watoto wenye uwezo wa kuwa viongozi katika nyanja mbalimbali kupata elimu bora kutoka vyuo vinavyotambulika kimataifa, hivyo inao mpango wa kutafuta ufadhili kwa wanafunzi wake.
Horton aliwataja waliobahatika kupata fursa hiyo kuwa ni Fatema Bhimani anayekwenda kusoma Chuo Kikuu cha Harvard; Angel Mcharo atakayekwenda Chuo Kikuu cha Duke, Elias Kalembo; Chuo Kikuu cha Yale, Lydia Nichols; Chuo Kikuu cha Washington vyote vya Marekani na Sakina Nazarali anayekwenda Chuo Kikuu cha Simon Fraser nchini Canada. Wengine ni Blaise Kramer atakayejiunga na Chuo Kikuu cha George Washington, Esuvat Bomani atakayekwenda Chuo Kikuu cha Cornell na Erik Ngoiya anayekwenda Chuo Kikuu cha Trinity, Marekani.
TIMIZA VIKOBA YAFIKIA VIKUNDI ZAIDI YA 70
Zaidi ya vikundi 70 vimejiandikisha na kuanza kunufaika huduma mpya ijulikanayo kama Timiza Vikoba iliyoanzishwa kwa ushirikiano kati ya Airtel na Benki ya Maendeleo.
Huduma hiyo ilianzishwa mwezi mmoja uliopita kwa lengo la kuviwezesha vikundi vya vikoba nchini kutumia njia ya kisasa na salama katika ukusanyaji wa michango, kutoa mikopo na marejesho ya mikopo.
Meneja kitengo cha Airtel Money, Moses Alphonce amesema mwitikio huo ni mkubwa na unaonyesha ni jinsi gani wateja wanavyofurahia huduma hizo za kibunifu zenye lengo la kuboresha mifumo yao ya kuweka na kukopa kuwa ya kisasa na rahisi zaidi.
“Mpaka sasa tuna zaidi ya vikundi 70 vimejisajiri na baadhi yao wameshaanza kukopa. mikopo ya takribani Sh5 milioni imeshatolewa,”amesema.





0 comments:
Post a Comment